Thursday, 28 May 2015

USHAURI KWA WANAOENDA KWENYE USAILI NA VYETI HALISI

Kutokana na watu wanaoenda kwenye usaili wa nafasi za kazi kutakiwa kwenda na vyeti halisi vya kitaaluma na vinginevyo, ipo haja ya kuchukua hatua kadhaa kwa usalama wa vyeti hivi.

Baadhi ya vyeti muhimu huwa havitolewi kwa mara ya pili na mamlaka husika endapo vitapotea (mfano vyeti vya NECTA vya zamani visivyo na picha). Hata vile ambavyo huwa vinatolewa mara ya pili, kama vya kuzaliwa na hati za matokeo ya vyuo, havipatikani kwa uharaka sana na labda mpaka vije kupatikana kunaweza kuwa na madhara ambayo yameshatokea ikiwemo muda na fedha.

Inashauriwa kuwa taarifa yoyote ya mawasiliano ya moja kwa moja na mhusika iliyoambatanishwa na vyeti hivyo halisi kama ambavyo nimeonesha mfano hapo juu.

Taarifa hii inaweza kuwa karatasi iliyoandikwa nambari ya simu, anuani pepe au kadi ya mawasiliano, maarufu kama 'business card'.

Nini umuhimu wa kufanya hivyo?

Kanuni za nyaraka zilizopotea zinapendekeza mtu aliyeokota vitu hivyo aviwasilishe ama kituo cha polisi au kwenye ofisi ambayo ilitoa nyaraka husika. Kutokana na utendaji hafifu wa Jeshi la Polisi, hasa katika mambo ambayo yanaonekana hayawagusi sana imekuwa ni vigumu mtu kufikishiwa nyaraka zilizopotea kwa muda, hata kama zitafika mikononi mwa jeshi hilo.

Mamlaka zinazohusika na utoaji wa nyaraka nazo haziko katika nafasi nzuri ya kumtafuta mhusika na kuhakikisha anafikishiwa amali zake kwa muda. Namna salama na rahisi ni kupitia mawasiliano ya moja kwa moja kati ya muokotaji na mpotelewaji wa nyaraka ni kupitia mawasiliano baina ya wawili hao ambayo yatawezekana endapo tu mpotelewa atakuwa amewezesha mawasiliano hayo.

NB: Kupotelewa kwa nyaraka kunaweza kuambatana na upotevu wa mali zingine ndogondogo, si vema kujaribu kumhisi msamaria mwema anayekutafuta ili akupatie nyaraka zako. Ni vema kuheshimu mchango wake kwako kwani thamani ya vyeti na nyaraka zako zilizopatikana hailingani na amali ulizopoteza.

Ahsanteni!
Share:

0 comments:

Post a Comment

Blog Archive